Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 13 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 7......



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Ni siku nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwa nguvu zetu wala si kwa uwezo wetu si kwamba sisi
tumetenda mema sana wala si kwa akili zetu wala utashi wetu
sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake Mungu ni kwa mapenzi yake Mungu wetu
sisi kuwa hivi tulivyo...
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati  wote
Asante kwa uwepo wako,pumzi,uzima,afya na kuwa tayari kwa 
majukumu yetu...
Utukuzwe ee Mungu wetu,Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni
wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho ni Alfa na Omega...!
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Mungu wetu....!!


Basi, ueni chochote kilicho ndani yenu ambacho ni cha kidunia: Uasherati, uchafu, shauku, tamaa mbaya na uchu (ambao ni sawa na kuabudu sanamu). Kwa sababu ya mambo hayo hasira ya Mungu huwajia wote wanaomwasi. Wakati mmoja nyinyi pia mliishi kufuatana na mambo hayo, mlipotawaliwa nayo. Lakini sasa mnapaswa kuachana na mambo haya yote: Hasira, tamaa na uovu; kufuru au maneno yasiyofaa yasitoke kamwe vinywani mwenu. Msiambiane uongo, kwani nyinyi mmekwisha vua ule utu wa kale pamoja na matendo yake yote, mkavaa utu mpya. Huu unaendelea kurekebishwa na Mungu, Muumba wake, kadiri ya mfano wake, ili mpate kumjua Mungu kwa ukamilifu. Katika hali hii, hakuna tena tofauti kati ya Mgiriki na Myahudi, aliyetahiriwa na asiyetahiriwa, msomi na asiye msomi, mtumwa na mtu aliye huru. Kristo ni kila kitu, na yumo katika yote.


Tazama jana imepita Mungu wetu Leo ni siku mpya Baba wa Mbinguni
na Kesho ni nyingine Jehovah...
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia
mikononi mwako..
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakutenda,kwakunena,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie katika majaribu Yahweh tunaomba utuokoe na yule
mwovu na kazi zake zote
Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona


Nyinyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo, basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe nyinyi. Zaidi ya hayo yote, zingatieni upendo, kwani upendo huunganisha kila kitu katika umoja ulio kamili. Nayo amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu; maana kwa ajili hiyo nyinyi mmeitwa katika mwili huo mmoja. Tena muwe na shukrani! Ujumbe wa Kristo na ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Imbeni Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Mungu mioyoni mwenu kwa shukrani. Na, kila mfanyacho kwa neno au tendo, fanyeni vyote kwa jina la Bwana Yesu na kumshukuru Mungu Baba kwa njia yake.

Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh tunaomba nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki 
wenye kuhitaji
Jehovah tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu
tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na vyote tunavyovimiliki
Jehovah ukatamalaki na kutuatamia Mungu wetu tukawe salama
rohoni,Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe macho ya kuona  Yahwweh
ukatupe masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za 
maisha yetu,Jehovah ukaonekane katika maisha yetu popote
tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Yahweh ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika miasha yetu
Hekima,busara, utu wema ukawe nasi na upendo ukadumu kati yetu
Yahweh ukatufanye barua njema nasi tukasomeke kama inavyokupendeza wewe....
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Enyi wake, watiini waume zenu, kwani ndivyo apendavyo Bwana. Nanyi waume, wapendeni wake zenu, na msiwe wakali kwao. Enyi watoto, watiini wazazi wenu daima maana hiyo humpendeza Bwana. Nanyi wazazi, msiwachukize watoto wenu, la sivyo watakata tamaa. Enyi watumwa, watiini wakuu wenu wa kidunia katika mambo yote, na si tu wakati wanapowatazama kwa kuwa mnataka kujipendekeza kwao; ila fanyeni hivyo kwa moyo wote, kwa sababu ya kumcha Bwana. Kila mfanyacho, fanyeni kwa moyo wote, kwa sababu ya Bwana na si kwa ajili ya mtu. Kumbukeni kwamba atawapeni tuzo lile alilowawekea watu wake. Mtumikieni Kristo Bwana! Atendaye mabaya atalipwa kufuatana na ubaya wake; Mungu hana ubaguzi.

Yahweh tunawaweka mikononi mwako wote 
wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani,Mungu wetu tuomba
ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na hitaji lake
Jehovah tunaomba ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako,
kusimamia Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie kulia kwao Mungu wetu tunaomba
ukawafute machozi yao
Jehovah ukaonekane katika maisha yao Yahweh tunaomba ukasikie,
ukapokee sala/maombi yetu Mungu wetu  ukawatendee sawasawa na
mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwanami/kunisoma
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na
mapenzi yake pendo lenu likadumu amani ya Kristo Yesu ikawe nanyi daima ....
Nawapenda.

1Elisha akamjibu, “Sikiliza neno la Mwenyezi-Mungu: Kesho wakati kama huu, humu Samaria kilo tatu za unga bora wa ngano zitagharimu fedha shekeli moja ya fedha, na kilo sita za shayiri kadhalika zitagharimu fedha shekeli moja.” 2Kapteni mwaminifu wa mfalme akamwambia Elisha, “Kama Mwenyezi-Mungu mwenyewe angefanya madirisha mbinguni, je, jambo hilo litawezekana!” Elisha akamjibu, “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini wewe hutakula.”

Jeshi la Aramu laondoka

3Kulikuwa na watu wanne wenye ugonjwa wa ukoma waliokuwa nje ya milango ya mji wa Samaria ambao walisemezana, wao kwa wao, “Mbona tunakaa hapa tukifa njaa? 4Hakuna maana ya kuingia mjini kwa sababu huko tutakufa. Kwa hiyo hebu twende kwenye kambi ya Waaramu; inawezekana wakatuua, au wasituue.” 5Hivyo, giza lilipoanza kuingia, wakaenda kwenye kambi ya Waaramu, lakini walipofika huko, hapakuwa na mtu. 6Maana Mwenyezi-Mungu alilifanya jeshi la Waaramu lisikie sauti kama ya jeshi kubwa lililokuwa na magari na farasi. Waaramu wakadhani kuwa mfalme wa Israeli amekodisha majeshi ya Wahiti na Wamisri kuja kuwashambulia. 7Basi, katika usiku huo, Waaramu walikimbia wote ili kuyaokoa maisha yao wakiacha mahema yao, farasi na punda wao, na hata kambi yao jinsi ilivyokuwa.
8Wakoma wale wanne walipofika pembeni mwa kambi, waliingia ndani ya hema moja, wakala na kunywa vile walivyopata humo, wakachukua fedha, dhahabu na nguo, wakaenda kuzificha. Wakaingia katika hema nyingine na kufanya vivyo hivyo. 9Lakini wakaambiana, “Tunalofanya si sawa! Hii ni habari njema tuliyo nayo leo, na ikiwa tutangoja mpaka asubuhi, bila shaka tutaadhibiwa. Twende mara moja tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme!” 10Hivyo, wakaondoka katika kambi ya Waaramu na kuwaita mabawabu wa mji na kuwaambia: “Tulikwenda katika kambi ya Waaramu na hatukuweza kumwona wala kumsikia mtu yeyote. Farasi na punda wangali wamefungwa, na mahema yako kama walivyoyaacha.”
11Walinda malango wakaeneza habari hizi mpaka zikafika nyumbani kwa mfalme. 12Ingawa kulikuwa bado giza, mfalme aliamka na kuwaambia maofisa wake, “Mimi najua mpango wa Waaramu! Wanajua tuna njaa mjini, sasa wameacha kambi yao kwenda kujificha ili tutakapokwenda kutafuta chakula, watukamate sote hai na kuuteka mji.”
13Mmoja kati ya maofisa wake akasema, “Watu wengi tayari wameangamia kama vile wale ambao wamekwisha fariki. Tafadhali utume watu wachache na farasi watano wa wale waliobaki ili waende kuona kumetokea nini.” 14Wakachagua watu na kuwapa magari mawili. Mfalme akawatuma kuwafuata Waaramu, akisema, “Nendeni mkaone.” 15Watu hao wakaenda mpaka Yordani na njiani waliona nguo na vifaa vingine Waaramu walivyoacha walipokuwa wanakimbia. Wakarudi na kumpasha mfalme habari. 16Watu wa Samaria wakatoka na kuteka nyara kambi ya Waaramu. Kama vile Mwenyezi-Mungu alivyosema: Kilo tano za unga safi wa ngano au kilo kumi za shayiri ziliuzwa kwa kipande kimoja cha fedha.
17Naye mfalme alikuwa amemweka ofisa mlinzi wake kulinda lango la mji. Ofisa huyo alikanyagwa papo hapo langoni na kuuawa na watu, kama vile Elisha mtu wa Mungu alivyotabiri wakati mfalme alipokwenda kumwona. 18Elisha alikuwa amemwambia mfalme kwamba wakati kama huo siku iliyofuata, kilo tano za unga mzuri wa ngano au kilo kumi za shayiri zingeuzwa kwa kipande kimoja cha fedha; lakini hapo awali 19kapteni alikuwa amembishia Elisha, akisema, “Kama Mwenyezi-Mungu mwenyewe angefanya madirisha mbinguni, je, jambo hili lingewezekana?” Naye Elisha alikuwa amemjibu, “Utaona yakitendeka, lakini chakula chenyewe hutakila.” 20Na hivyo ndivyo ilivyotokea – kapteni akafa kwa kukanyagwa na watu kwenye lango la mji.



2Wafalme7;1-20


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: