Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 6 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalem 2......



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye huruma,Mungu wa walio hai
Mungu mwenye kuponya,Mungu mwenye kubariki,Mungu mwenye kusamehe
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Jehovah Jire,Jehovah Nissi,Jehovah Shammah,Jehovah Shalom,Emanuel-Mungu pamoja nasi...!!

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu...!!!


Ndugu zangu, wengi wenu msiwe waalimu. Kama mjuavyo, sisi waalimu tutapata hukumu kubwa zaidi kuliko wengine. Lakini kama mtu hakosi katika usemi wake, basi, huyo ni mkamilifu, na anaweza kutawala nafsi yake yote. Sisi huwatia farasi lijamu kinywani mwao ili watutii; na kwa njia hiyo twaweza kuwaongoza kokote tunakotaka. Meli nazo pia, ingawa ni kubwa sana, na husukumwa na upepo mkali, huweza kugeuzwa kwa usukani mdogo sana, zikaelekea kokote nahodha anakotaka. Vivyo hivyo, ulimi, ingawa ni kiungo kidogo cha mwili, hujisifia makuu sana. Moto mdogo waweza kuteketeza msitu mkubwa.

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia
mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhamabi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Baba wa Mbinguni usitutie katika majaribu Mungu wetu tunaomba 
utuokoe na  yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti 
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Hali kadhalika ulimi ni kama moto. Umejaa maovu chungu nzima, unayo nafasi yake katika miili yetu na hueneza ubaya katika nafsi zetu zote. Huteketeza maisha yetu yote kwa moto utokao Jehanamu kwenyewe. Binadamu anaweza kuwafuga wanyama, na amefaulu kufuga viumbe vyote – wanyama wa mwituni, ndege, nyoka na viumbe vya baharini. Lakini hakuna mtu aliyefaulu kuufuga ulimi. Ulimi ni kitu kiovu, hakitawaliki, na kimejaa sumu inayoua. Kwa ulimi sisi twamshukuru Bwana na Baba yetu. Kwa ulimi huhuo twawalaani watu, watu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu. Maneno ya kubariki na ya kulaani hutoka katika kinywa kimoja. Ndugu zangu, mambo haya hayapaswi kuwa hivyo. Je, chemchemi moja yaweza kutoa maji matamu na maji machungu pamoja? Ndugu zangu, je, mtini waweza kuzaa zeituni? Au, mzabibu waweza kuzaa tini? Chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Yahweh tunaomba
ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende
sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Yahweh ukatupe kama
inavyokupendeza wewe....

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Jehovah tunaomba
ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni
ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo...
Yahweh ukatamalaki na kutuatamia,Mungu wetu tukawe salama rohoni
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia
sauti yako na kuitii,Yahweh tunaomba ukatuguse kwa mkono wako wenye
nguvu,Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Jehovah tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za 
maisha yetu,Yahweh ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni,Neema yako na Nuru yako
ikaangaze katika maisha yetu,amani yako ikatawale na upendo ukadumu kati yetu...
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi.....

Je, ni nani mwenye hekima na akili miongoni mwenu? Basi, aoneshe jambo hilo kwa mwenendo wake mzuri na kwa matendo yake mema yanayofanyika kwa unyenyekevu na hekima. Lakini ikiwa mioyo yenu imejaa wivu, chuki na ubinafsi, basi, msijisifu na kusema uongo dhidi ya ukweli. Hekima ya namna hiyo haitoki juu mbinguni; hekima hiyo ni ya ulimwengu, na ya kidunia, tena ni ya kishetani. Maana popote palipo na wivu na ubinafsi, hapo pana fujo na kila aina ya uovu. Lakini hekima itokayo juu mbinguni, kwanza ni safi; inapenda amani, upole na huwajali watu; imejaa huruma na huzaa matunda ya matendo mema; haina ubaguzi wala unafiki. Uadilifu ni mazao ya mbegu ambazo wapenda amani hupanda katika amani.

Yahweh tazama watoto wako wanaokutafuta kwa bidii/imani
mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawatendee kila mmoja na mahitaji yake
Jehovah tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu tunaomba ukawape neema ya kufuata njia zako nazo zikawaweke huru
Mafalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yao
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yao Baba wa Mbinguni
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao Jehovah tunaomba ukasikie
kulia kwao Mungu wetu tunaomba ukawafute machozi yao
Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie,ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu tunaomba ukawajibu sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa/waungana kwakuwa nami/kunisoma
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na
mapenzi yake,Amani ya Kristo Yesu na upendo wa Mungu Baba 
ukawawe nanyi Daima...
Nawapenda

Elia anachukuliwa mbinguni

1Ikawa wakati ulipofika ambapo Mwenyezi-Mungu alitaka kumchukua Elia mbinguni katika upepo wa kisulisuli, Elia na Elisha walikuwa njiani, wakitoka Gilgali. 2Baadaye walipokuwa njiani, Elia alimwambia Elisha, “Tafadhali wewe kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende Betheli.”
Lakini Elisha akamwambia, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo, sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja hadi Betheli. 3Wanafunzi wa manabii waliokuwa huko wakamwendea Elisha, wakamwuliza, “Je, unajua kwamba leo Mwenyezi-Mungu atamchukua bwana wako?” Elisha akajibu, “Naam! Najua; nyamazeni.”
4Elia akamwambia Elisha, “Tafadhali kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende Yeriko.” Lakini Elisha akakataa akisema, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja mpaka Yeriko.
5Wanafunzi wa manabii huko Yeriko wakamwendea Elisha na kumwuliza, “Je, unajua kwamba hivi leo Mwenyezi-Mungu atamchukua bwana wako?” Elisha akawajibu, “Naam! Najua; nyamazeni.”
6Kisha Elia akamwambia Elisha, “Tafadhali wewe kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende mtoni Yordani.” Lakini Elisha akasema, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja. 7Manabii hamsini wakawafuata mpaka mtoni Yordani. Elia na Elisha wakasimama karibu na mto, nao manabii wakasimama mbali kidogo. 8Elia akalivua vazi lake, akalikunja na kuyapiga maji, maji yakagawanyika katika sehemu mbili, nao wakavuka hadi ngambo ya pili, wakapitia mahali pakavu. 9Walipofika ngambo, Elia akamwambia Elisha, “Niambie unalotaka nikufanyie kabla sijaondolewa kwako.” Elisha akamwambia, “Naomba sehemu maradufu ya roho yako.” 10Elia akajibu, “Ombi lako ni gumu, hata hivyo utakipokea kipawa changu hicho ikiwa utaniona wakati nitakapoondolewa kwako; lakini usiponiona, basi hutapewa.” 11Walipokuwa wanatembea na kuongea, ghafla, gari la moto likatokea pamoja na farasi wa moto; likawatenganisha; naye Elia akachukuliwa mbinguni katika kisulisuli. 12Elisha alipoona tukio hilo akalia, “Baba yangu, baba yangu! Gari la Israeli na wapandafarasi wake!” Basi, Elisha hakumwona tena Elia.
Ndipo Elisha alipoyashika mavazi yake na kuyararua vipande viwili. 13Kisha akaliokota vazi la Elia lililomwangukia, akarudi na kusimama ukingoni mwa mto Yordani. 14Akayapiga maji kwa vazi la Elia akisema, “Yuko wapi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Elia?” Alipoyapiga maji, yakagawanyika sehemu mbili, naye akavuka hadi ngambo.
15Wale wanafunzi wa manabii kutoka Yeriko walipomwona, walisema, “Roho ya Elia iko kwa Elisha.” Basi, wakaenda kumlaki, wakasujudu mbele yake. 16Wakamwambia, “Sisi watumishi wako tunao mashujaa hamsini; tafadhali waruhusu waende kumtafuta bwana wako. Ikiwa roho ya Mwenyezi-Mungu imembeba na kumtupa juu ya mlima fulani au bondeni.” Elisha akajibu, “La, msiwatume.”
17Lakini wao waliposisitiza mpaka akaona haya, aliwaambia “Watumeni.” Hivyo wakawatuma watu hamsini, wakaenda wakamtafuta kila mahali kwa muda wa siku tatu wasimwone. 18Kisha wakarudi kwa Elisha aliyekuwa anawangojea huko Yeriko. Elisha akawauliza, “Je, sikuwaambieni msiende?”

Miujiza ya Elisha

19Baadaye watu wa Yeriko walimwendea Elisha, wakamwambia, “Bwana, kama uonavyo mji huu ni mzuri, lakini maji tuliyo nayo ni mabaya na yanasababisha mimba kuharibika.”
20Elisha akawaambia, “Tieni chumvi ndani ya bakuli jipya, kisha mniletee.” Nao wakamletea. 21Elisha akaenda kwenye chemchemi ya maji, akatupa chumvi hiyo ndani na kusema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimeyafanya maji haya kuwa yenye kufaa; tangu sasa hayatasababisha vifo au kutoa mimba.” 22Na maji hayo yamekuwa ya kufaa mpaka leo, kama alivyosema Elisha. 23Elisha aliondoka Yeriko, akaenda Betheli. Alipokuwa njiani, vijana fulani walitoka mjini wakaanza kumzomea wakisema, “Nenda zako, nenda zako mzee kipara!” 24Elisha aligeuka akawatazama na kuwalaani kwa jina la Mwenyezi-Mungu. Dubu wawili majike wakatoka mwituni, wakawararua vijana arubaini na wawili miongoni mwao.
25Elisha akaendelea na safari yake mpaka mlima Karmeli na kutoka huko akarudi Samaria.



2Wafalme2;1-25


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: