Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 5 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 32 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu na Muumba wa vyote...
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Baba wa upendo,Baba wa Baraka,Mfalme wa Amani..
Yahweh,Jehovah,El shaddai,Elo him,El Olam,El Qanna,Emanuel..
Mungu pamoja nasi..!!
Utukuzwe Jehovah,Uhimidiwe Yahweh,Usifiwe Mungu wetu..
Uabudiwe Baba wa Mbinguni,Hakuna kama wewe..
wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Alfa na Omega..
Unatosha Mungu wetu,Matendo yako ni ya ajabu...
Matendo yako ni makuu mno...!!



Sasa, ndugu, napenda kuwakumbusha ile Habari Njema niliyowahubirieni, nanyi mkaipokea na kusimama imara ndani yake. Kwa njia yake mnaokolewa, ikiwa mnayazingatia maneno niliyowahubirieni, na kama kuamini kwenu hakukuwa bure. Mimi niliwakabidhi nyinyi mambo muhimu sana ambayo mimi niliyapokea: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na Maandiko Matakatifu; kwamba alizikwa, akafufuka siku ya tatu kufuatana na Maandiko Matakatifu; kwamba alimtokea Kefa, na baadaye aliwatokea wale kumi na wawili. Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya 500 kwa mara moja; wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa. Baadaye alimtokea Yakobo kisha akawatokea mitume wote. Baada ya wote, akanitokea hata mimi, mimi niliyekuwa kama mtu aliyezaliwa kabla ya wakati. Maana mimi ni mdogo kabisa miongoni mwa mitume, na wala sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililidhulumu kanisa la Mungu. Lakini, kwa neema yake Mungu, nimekuwa kama nilivyo, na neema yake kwangu haikuwa bure. Mimi nimefanya kazi kuliko wote; si mimi hasa, ila ni neema ya Mungu ifanyayo kazi pamoja nami. Lakini hata hivyo, iwe wao ndio wahubirio au mimi nihubiriye, haidhuru, hiki ndicho tunachohubiri, na hiki ndicho mnachoamini.

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii..
Si kwamba sisi ni wema sana,wala si kwamba sisi ni wazuri mno
Si kwa nguvu zetu wala uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo..
Ni kwa mapenzi yako,nikwa Neema na rehema zako Mungu wetu

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Baba tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu
 na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote...
Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
na utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..




Sasa, maadamu inahubiriwa kwamba Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, baadhi yenu wanawezaje kusema kwamba hakuna ufufuo wa wafu? Kama hakuna ufufuo wa wafu, basi, Kristo naye hakufufuka; na kama Kristo hakufufuka, basi mahubiri yetu hayana maana na imani yenu haina maana. Zaidi ya hayo sisi tungekuwa mashahidi wa uongo mbele ya Mungu, maana tulisema kwamba Mungu alimfufua Kristo kutoka kwa wafu na kumbe yeye hakumfufua – kama ni kweli kwamba wafu hawafufuliwi. Maana, ikiwa ni kweli kwamba wafu hawafufuki, basi naye Kristo hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuliwa, basi, imani yenu ni ya bure; mngali bado katika dhambi zenu. Zaidi ya hayo, wale wote waliokufa wakiwa wameungana na Kristo wamepotea kabisa. Kama matumaini yetu katika Kristo yanahusu tu maisha haya ya sasa, basi, sisi ni watu wa kusikitikiwa zaidi kuliko wengine wote duniani. Lakini ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, wa kwanza wa wale waliolala katika kifo. Maana kama vile kifo kilivyoletwa duniani na mtu mmoja, vivyo hivyo nako kufufuka kutoka kwa wafu kumesababishwa na mtu mmoja. Kama vile watu wote wanavyokufa kwa kujiunga na Adamu, vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo. Lakini kila mmoja kwa mpango wake: Kristo kwanza; halafu wale walio wake Kristo wakati Kristo atakapokuja. Baada ya hayo, mwisho utafika wakati ambapo Kristo atamkabidhi Mungu Baba ufalme, baada ya kufutilia mbali kila tawala na mamlaka na nguvu. Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda maadui zake wote na kuwaweka chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni kifo. Maana, Maandiko yasema: “Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini, Maandiko yanaposema: “Vitu vyote vimewekwa chini ya miguu yake avitawale” ni dhahiri kwamba Mungu haingii katika kundi hilo la vitu, maana yeye ndiye anayeviweka vitu hivyo chini ya Kristo. Lakini vitu vyote vitakapowekwa chini ya utawala wa Kristo, ndipo naye Mwana atakapojiweka chini ya Mungu, aliyeweka vyote chini ya utawala wake; ili Mungu atawale juu ya vyote. Kama hakuna ufufuo, je watu wale wanaobatizwa kwa ajili ya wafu wanatumainia kupata nini? Kama wafu hawafufuliwi, ya nini kubatizwa kwa ajili yao? Na sisi, ya nini kujitia hatarini kila saa? Ndugu, mimi nakikabili kifo kila siku! Fahari niliyo nayo juu yenu katika kuungana na Kristo Yesu Bwana wetu inanifanya nitangaze jambo hili. Kama kusudi langu lingalikuwa la kibinadamu tu, kule kupigana kwangu na wanyama wakali hapa Efeso kungalinifaa kitu gani? Kama wafu hawafufuki, basi, “Tule na tunywe, maana kesho tutakufa.” Msidanganyike! Urafiki mbaya huharibu tabia njema. Amkeni! Anzeni kuishi vema, na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hawamjui Mungu kabisa. Hii nawaambieni, ni aibu kubwa kwenu!



Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Biashara,
Masomo na yote tunayoenda kufanya/kutenda tukatende
sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo,Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema
ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu..
Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa Amani tuyaweka maisha yetu mikononi mwako..
Nyumba/Ndoa zetu,watoto,wazazi,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako,Furaha,Amani yako ikatawale..
Upendo ulio wako,hekima,busara na tukanene yaliyo yako..
Tukasimamie Neno lako Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..



Lakini mtu anaweza kuuliza: “Wafu watafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” Hayo ni maswali ya kijinga! Ukipanda mbegu, isipokufa kwanza haitaota. Unachopanda ni mbegu tu, labda ya ngano au nafaka nyingine, na si mmea mzima ambao hutokea baadaye. Mungu huipa hiyo mbegu mwili anaoutaka mwenyewe; kila mbegu hupata mwili wake wa pekee. Miili ya viumbe vyote si sawa. Miili ya binadamu ni ya namna moja, ya wanyama ni ya namna nyingine, ya ndege ni ya namna nyingine na miili ya samaki pia ni ya namna nyingine. Iko miili ya mbinguni na miili ya duniani; uzuri wa miili ya mbinguni ni mwingine, na uzuri wa miili ya duniani ni mwingine. Uko uzuri wa jua, wa mwezi na wa nyota; hata nyota nazo huhitilafiana kwa uzuri. Ndivyo ilivyo kuhusu ufufuo wa wafu. Kama vile mbegu, mwili huzikwa ardhini ukiwa katika hali ya kuharibika, lakini hufufuliwa katika hali ya kutoharibika. Huzikwa katika hali duni, hufufuliwa katika hali tukufu; huzikwa katika hali dhaifu, hufufuliwa ukiwa wenye nguvu. Unapozikwa ni mwili wa kawaida, unapofufuliwa ni mwili wa kiroho. Kuna mwili wa kawaida na kutakuwa na mwili wa kiroho. Maana Maandiko yasema: “Mtu wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe mwenye uhai;” lakini Adamu wa mwisho ni Roho awapaye watu uhai. Lakini unaotangulia kuwako si ule mwili wa kiroho, ila ule mwili wa kawaida, kisha ule mwili wa kiroho. Adamu wa kwanza aliumbwa kwa udongo, alitoka ardhini; mtu wa pili alitoka mbinguni. Wote walio wa dunia wako kama huyo mtu aliyeumbwa kwa udongo; wale walio wa mbinguni wako kama yule aliyetoka mbinguni. Kama vile tulivyofanana na yule aliyeumbwa kwa udongo, vivyo hivyo tutafanana na huyo aliyetoka mbinguni.

Yahweh tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa..
waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye mashaka/hofu..
walioanguka na kuelemewa na mizigo,walio katika vifungo vya 
yule mwovu na wote wenye kuhitaji..
Mungu wetu tunaomba unyooshe mkono wako wenye nguvu...
ukawaguse na kuwaponya kimwili na kiroho pia..
Baba wa Mbinguni ukawafungue na wakapate kuwa huru..
Yahweh ukawasimamishe na kuwasamehe wale waliokwenda kinyume nawe..
Baba wa Mbimnguni ukawape neema ya kujiombea ,Mfalme wa Amani Nuru yako ikaangaze katika maisha ya watoto wako..
Baba ukasikie kulia kwao Jehovah ukawafute machozi yao
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yao..
Yahweh ukawape neema ya kukujua wewe na kusimamia
Neno lako na wakafuate njia zako nao wakapate kuwa huru..
Wafiwa ukawe mfariji wao..



Basi, ndugu, nasema hivi: Kile kilichofanywa kwa mwili na damu hakiwezi kuushiriki ufalme wa Mungu; na chenye kuharibika hakiwezi kuwa na hali ya kutoharibika. Sikilizeni, nawaambieni siri: Sisi hatutakufa sote, ila sote tutageuzwa, wakati wa mbiu ya mwisho, kwa nukta moja, kufumba na kufumbua. Maana tarumbeta ya mwisho itakapolia, wafu watafufuliwa katika hali ya kutoweza kufa tena, na sisi tutageuzwa. Maana ni lazima kila kiharibikacho kijivalie hali ya kutoharibika, mwili uwezao kufa ujivalie hali ya kutokufa. Basi, mwili huu wenye kuharibika utakapojivalia hali ya kutoharibika, na kile chenye kufa kitakapojivalia hali ya kutokufa, hapo ndipo litakapotimia lile neno lililoandikwa: “Kifo kimeangamizwa; ushindi umekamilika!” “Kifo, ushindi wako uko wapi? Uwezo wako wa kuumiza uko wapi?” Kifo hupata sumu yake katika dhambi, nayo dhambi hupata nguvu yake katika sheria. Lakini tumshukuru Mungu anayetupatia ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu zangu wapenzi, simameni imara na thabiti. Endeleeni daima kuwa na bidii katika kazi ya Bwana, mkijua kwamba kazi mnayofanya katika utumishi wa Bwana haitapotea bure.

Jehovah tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Tukishukuru na kuamini wewe ndiye Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!
Wapendwa/waungwana asanteni sana kwakuwa nami..
Baba wa faraja,upendo,Amani awe nanyi 
Nuru yake ikaangaze katika maisha yenu..
Nawapenda.


1“Tegeni masikio enyi mbingu:
Sikiliza, ee dunia, maneno ninayosema.
2Mafundisho yangu na yatone kama mvua,
maneno yangu yadondoke kama umande,
kama manyunyu kwenye mimea michanga,
kama mvua nyepesi katika majani mabichi.
3Maana nitalitangaza jina la Mwenyezi-Mungu,
nanyi mseme, ‘Mungu wetu ni Mkuu’.
4“Mwenyezi-Mungu ni Mwamba wa usalama;
kazi zake ni kamilifu,
njia zake zote ni za haki.
Yeye ni Mungu mwaminifu asiye na kosa,
yeye hufanya mambo ya uadilifu na ya haki.
5Lakini nyinyi mmekosa uaminifu kwake,
nyinyi sio watoto wake tena kwa sababu ya uovu,
nyinyi ni kizazi kiovu na kipotovu.
6Mnawezaje kumlipa hivyo Mwenyezi-Mungu,
enyi watu wapumbavu na msio na akili?
Je, yeye siye Baba yenu aliyewaumba,
aliyewafanya na kuwaimarisha?
7Kumbukeni siku zilizopita,
fikirieni miaka ya vizazi vingi;
waulizeni baba zenu nao watawajulisha,
waulizeni wakubwa wenu nao watawaeleza.
8Mungu Mkuu alipoyagawia mataifa mali yao,
alipowagawa wanadamu,
kila taifa alilipatia mipaka yake,
9kulingana na idadi ya watoto wa Mungu,32:9 watoto wa Mungu: Tafsiri kadiri ya hati ya Kumrani. Kiebrania: Watoto wa Israeli.
lakini alijiwekea watu wa Yakobo kuwa wake,
hao alijichagulia kuwa mali yake.
10Aliwakuta katika nchi ya jangwa,
nyika tupu zenye upepo mkali.
Aliwalinda na kuwatunza,
aliwafanya kama mboni ya jicho lake.
11Kama tai alindaye kiota chake,
na kurukaruka juu ya makinda yake,
akitandaza mabawa yake ili kuwashikilia,
na kuwabeba juu ya mabawa yake.
12Yeye Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwaongoza
na hapakuwa na mungu mwingine wa kumsaidia.
13Aliwapitisha katika nyanda za juu za nchi,
nao wakala mazao ya mashambani.
Akawapa asali miambani waonje
na mafuta kutoka mwamba mgumu.
14Aliwapa siagi na maziwa ya mifugo,
mafuta ya wanakondoo na kondoo madume,
makundi ya mifugo ya Bashani na mbuzi.
Aliwapa ngano nzuri kabisa na divai mpya wakanywa.
15Watu wa Israeli walinona na kupiga mateke;
walinenepa, wakawa na kitambi na kunawiri;
kisha wakamwacha Mungu aliyewaumba,
wakamdharau Mwamba wa wokovu wao.
16Walimfanya aone wivu mkali kwa miungu yao,
walimchochea akasirike kwa matendo yao ya kuchukiza.
17Walitambikia majini ambayo hayakuwa miungu,
waliiendea miungu ambayo hawakuijua kamwe,
miungu mipya iliyotokea siku za karibuni,
ambayo wazee wao hawakuiheshimu kamwe.
18Hamkumjali Mwamba aliyewapa uhai,
mlimsahau Mungu aliyewazaa nyinyi.
19Mwenyezi-Mungu aliona jambo hilo akawaacha;
aliwakataa watoto wake, waume kwa wake.
20Akasema, ‘Nitawaficha uso wangu
nione mwisho wao utakuwaje!
Maana wao ni kizazi kipotovu,
watoto wasio na uaminifu wowote.
21Wamenichochea kuona wivu kwa kitu kisicho mungu,
wamenikasirisha kwa sanamu zao.
Hivyo nitawafanya waone wivu kwa kisicho watu,
nitawakasirisha kwa kutumia taifa la wapumbavu.
22Hasira yangu imewaka moto,
inachoma mpaka chini kuzimu,
itateketeza dunia na vilivyomo,
itaunguza misingi ya milima.
23Nitarundika maafa chungu nzima juu yao,
nitawamalizia mishale yangu.
24Watakonda kwa njaa,
wataangamizwa kwa homa kali.
Nitapeleka wanyama wenye meno makali kuwashambulia,
na nyoka wenye sumu wanaotambaa mavumbini.
25Vita vitasababisha vifo vingi nje
na majumbani hofu itawatawala,
vijana wa kiume na wa kike watauawa
hata wanyonyao na wazee wenye mvi.
26Nilisema, ningaliwaangamiza kabisa
na kuwafanya wasikumbukwe tena na mtu yeyote,
27ila tu kwa sababu ya majivuno ya maadui zao
ili maadui zao wasije wakafikiria vingine;
wasije wakasema, wamefaulu kuwaangamiza,
nami Mwenyezi-Mungu sihusiki katika mambo haya!’
28“Israeli ni taifa lisilo na akili,
watu wake hawana busara ndani yao.
29Wangekuwa na hekima wangejua kwa nini walishindwa,
wangeweza kuelewa mwisho wao utakuwaje.
30Mtu mmoja anawezaje kuwashinda watu 1,000,
au watu wawili wanawezaje kuwashinda watu 10,000,
isipokuwa kama Mwamba wao amewatupa,
Mwenyezi-Mungu wao amewaacha?
31Hata adui zetu wenyewe wamekiri wazi,
mwamba wao hauna nguvu kama mwamba wetu.
32Maana mizabibu yao ni miche ya Sodoma
zimetoka katika konde za Gomora;
zabibu zake ni zabibu zenye sumu,
vishada vyake ni vichungu.
33Divai yao ni kama sumu ya nyoka,
ina sumu kali ya majoka.
34“Je sina njia ya kuwaadhibu?
Silaha zangu ninazo mkononi.
35Kisasi ni juu yangu,
mimi nitalipiza,
wakati miguu yao itakapoteleza;
maana siku yao ya maafa imewadia,
mwisho wao u karibu sana.
36Mwenyezi-Mungu atawatetea watu wake,
na kuwahurumia watumishi wake,
wakati atakapoona nguvu zao zimeishia,
wala hakuna aliyebaki, mfungwa au mtu huru.
37Ndipo Mwenyezi-Mungu atakapowauliza watu wake,
‘Iko wapi ile miungu yenu,
mwamba mlioukimbilia usalama?’
38Iko wapi hiyo miungu iliyokula matoleo yenu
na kunywa divai na tambiko zenu za kinywaji?
Basi na iinuke, iwasaidieni;
acheni hiyo iwe kinga yenu sasa!
39Oneni kuwa mimi ndimi Mungu
na wala hakuna mwingine ila mimi.
Mimi huua na kuweka hai;
hujeruhi na kuponya,
na hakuna awezaye kumwokoa yeyote mikononi mwangu.
40Nanyosha mkono wangu mbinguni,
na kuapa, kwa uhai wangu wa milele,
41kama mkiuona upanga wangu umeremetao,
na kunyosha mkono kutoa hukumu,
nitawalipiza kisasi maadui zangu,
nitawaadhibu wale wanaonichukia.
42Mishale yangu nitailevya kwa damu,
upanga wangu utashiba nyama,
utalowa damu ya majeruhi na mateka
na adui wenye nywele ndefu.
43“Enyi mataifa washangilieni watu wake,
maana yeye hulipiza kisasi damu ya watumishi wake,
huwalipiza kisasi wapinzani wake,
na kuitakasa nchi ya watu wake.”
44Mose alikuja mbele ya Yoshua, mwana wa Nuni, wakakariri maneno ya wimbo huu, ili Waisraeli wote wausikie.

Wosia wa Mose

45Mose alipomaliza kuwaambia watu wa Israeli maneno haya yote, 46aliwaambia, “Yawekeni mioyoni mwenu maneno yote ambayo ninawapeni leo. Lazima muwaamuru watoto wenu ili wafuate kwa uaminifu maneno yote ya sheria hii. 47Maana sheria hii si maneno matupu bali ni uhai wenu; kwa sheria hii mtaishi maisha marefu katika nchi mnayokwenda kuimiliki, ngambo ya mto Yordani.”
48Siku hiyohiyo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 49“Panda mlima huu wa Abarimu, mlima Nebo katika nchi ya Moabu, mkabala wa mji Yeriko, ukaiangalie nchi ya Kanaani ninayowapa Waisraeli waimiliki. 50Kisha ufariki hukohuko mlimani kama kaka yako Aroni alivyofariki katika mlima Hori, 51kwa sababu nyote wawili mlivunja uaminifu wenu kwangu mbele ya Waisraeli mlipokuwa kwenye maji ya Meriba, karibu na mji wa Kadeshi, katika jangwa la Sini, mkakosa kuuthibitisha utakatifu wangu kati ya Waisraeli. 52Utaiona nchi iliyo mbele yako, lakini hutaingia katika nchi hiyo ninayowapa Waisraeli.”



Kumbukumbu la Sheria 32:1-52

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: