Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 20 April 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 16...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Mungu wetu ni mwema sana Tumshukuru kwa yote...

Ni nani aliye mkuu?
(Mat 18:1-5; Marko 9:33-37)
46Kukatokea majadiliano kati ya wale wanafunzi kuhusu nani kati yao aliyekuwa mkuu zaidi. 47Yesu aliyajua mawazo yaliyokuwa mioyoni mwao; basi akamchukua mtoto mdogo akamweka karibu naye, 48akawaambia, “Mtu yeyote anayempokea mtoto huyu mdogo kwa jina langu, ananipokea mimi; na yeyote anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma. Maana yule aliye mdogo kuliko wote kati yenu ndiye aliye mkuu kuliko wote.”[Luka 9:46-48]
Asante Baba wa mbinguni kwa Neema/Rehema yako na  kutuchagua sisi tena na kutupa Kibali cha  kuiona Leo hii, Sisi ni nani Baba..? Si kwamba ni wazuri mno,Si kwamba ni wema sana zaidi ya wengine,si kwamba tunajua sana, si kwamba tunanguvu na utashi..si kwamba hatukosei Jehovah..!! Bali ni kwa Mapenzi yako Mungu wetu...

Tunashukuru na tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza na kukabidhi maisha yetu mikononi mwako Yahweh..!!
Tunaomba Baba utubariki tuingiapo/tutokapo,vinywaji/vilaji,vyombo vya usafiri na tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Yahweh..!!
Ukabariki Kazi zetu,Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia ukavitakase kwa Damu ya mwanao mpendwa Bwana wetu na mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..Yeye aliteseka ili sisi tupate kupona..
Ukatutakase miili yetu na Akili zetu,Roho mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda,kutambua/kujitambua ..

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe..
Tunakwenda kinyume na mwovu na kazi zake zote..
Tunaomba utupe Neema ya kuweza kusameheana pia..
Utuokoe, Ututakase na kutufunika na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Tukawe chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yako..

Baba wa Mbinguni tunawaweka  mikononi mwako wenye Shida/Tabu, wagonjwa,wanaopitia magumu/majaribu,waliovifungoni,waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye mashaka/hofu,wasiojiweza,Yatima na wajane,Baba ukawaguse naukawaponye, kimwili na kiroho, wakauone Utukufu wako Jehovah..!

Baba usiwaache na ukawaguse na kuwapatia Mke/Mume mwema wote wanaotafuta wenza wao ili wapate kujenga familia iliyo bora na kukujua wewe..
Tazama wanaotafuta watoto pia Mungu ukawape watoto na wawe wema, wakujue wewe Mungu na wakawe baraka kwa wazazi/walezi na jamii pia..

Tazama kuna wanaohitaji kwenda shule Baba wa Mbinguni lakini kunavifungo mbalimbali , wengine wamefiwa na wanaowasomesha, wengine hali ya pesa haiko vyema, wengine hawaelewi/hawakumbuki wanayofundishwa, wengine wanapofika shuleni wanakuwa wagonjwa na mengine meengi Baba wa Mbingu hakuna mtatuzi wa haya zaidi yako Mungu wetu.. tunayaweka mikononi mwako wewe uwezaye yote hakuna litaloshindikana kwako Baba wa mbinguni..Tuna amini na kukuabudu daima..!! Wewe ukisema ndiyo hakuna wakusema siyo.. Maana wewe ni Baba wa Upendo, Baba wa Yatima, Mume wa Wajane,Mungu wetu na Muumba wetu,hakuna  na hata kuwepo wala wa kufanana nawe Jehovah..
Maisha yetu pasipo wewe ni bure kabisa..Unatosha Baba wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho..wewe ni Afla na Omega..!!
Tunayakidhi haya yote tuliyoyanena na tunayoyawaza Baba yote unayajua..Tukiamini na kushukuru..
Amina..!!
Nawapenda wote na mliopita hapa Mungu aendelee kuwabariki Asanteni sana..
Neno litasimama mambo yote yatapita lakini Neno litasimama..!!

Mana na kware

1Jumuiya yote ya Waisraeli iliondoka, ikafika jangwa la Sini kati ya Elimu na Sinai. Hii ilikuwa siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili tangu walipoondoka nchini Misri. 2Basi, jumuiya yote ya Waisraeli ikawalalamikia Mose na Aroni huko jangwani, 3“Laiti Mwenyezi-Mungu angelituua tulipokuwa nchini Misri ambako tulikaa, tukala nyama na mikate hata tukashiba. Lakini nyinyi mmetuleta huku jangwani kuiua jumuiya hii yote kwa njaa!”
4 Taz Hek 16:20-29; Yoh 6:31 Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mimi nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Kila siku watu watatoka na kukusanya chakula cha siku hiyo. Kwa njia hii nitawajaribu nione kama watazifuata sheria zangu au hawatazifuata. 5Lakini siku ya sita, wakati watakapoandaa chakula walichokusanya, kiasi hicho kitakuwa mara mbili ya chakula cha kila siku.” 6Basi, Mose na Aroni wakawaambia watu wote wa Israeli, “Jioni, mtatambua kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye aliyewatoa nchini Misri! 7Tena, kesho asubuhi, mtauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu kwani ameyasikia manunguniko mliyomnungunikia. Sisi ni nani hata mtunungunikie?” 8Tena Mose akasema, “Jioni, Mwenyezi-Mungu atawapeni nyama mle, na asubuhi atawapeni mikate mle mshibe, maana yeye ameyasikia manunguniko mliyomnungunikia. Sisi ni nani hata mtunungunikie? Msitunungunikie sisi bali mnungunikieni Mwenyezi-Mungu.”
9Kisha Mose akamwambia Aroni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli ikusanyike mbele ya Mwenyezi-Mungu kwani ameyasikia manunguniko yenu.” 10Wakati Aroni alipokuwa akizungumza na jumuiya ya Waisraeli, watu wote walitazama huko jangwani, na mara utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukaonekana mawinguni. 11Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 12“Nimeyasikia manunguniko ya Waisraeli. Basi, waambie kwamba wakati wa jioni watakula nyama, na asubuhi watakula mkate. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”
13Basi, mnamo wakati wa jioni kukaja kware wengi, wakafunika kambi ya Waisraeli. Asubuhi yake kukatokea umande, ukatanda kandokando ya kambi yao. 14Umande huo ulipotoweka, kukabaki huko nyikani kitu kama mkate mwembamba na mwepesi. 15Taz 1Kor 10:3 Waisraeli walipoona kitu hicho walishangaa, wakaulizana, “Nini hiki?”16:15 Nini hiki: Kiebrania: Man-hu. Hawakujua kilikuwa kitu gani. Basi, Mose akawaambia, “Huu ni mkate ambao Mwenyezi-Mungu amewapa mle. 16Mwenyezi-Mungu ameamuru mfanye hivi: Kila mtu na akusanye chakula kiasi anachoweza kula; ataokota kiasi cha pishi16:16 pishi: Kiebrania: Omeri; Taz Kut 16:36. moja kwa kila mtu hemani mwake.”
17Basi, Waisraeli wakafanya hivyo, na ikawa kwamba, wengine waliokota kwa wingi na wengine kidogo. 18Taz 2Kor 8:15 Lakini wote walipokipima kipimo walichookota katika pishi, waligundua kuwa aliyeokota kingi hakuwa na cha ziada, na aliyeokota kidogo, hakupungukiwa. Kila mmoja alikuwa ameokota kiasi alichoweza kula.
19Mose akawaambia watu, “Mtu yeyote asibakize chakula hicho mpaka asubuhi.”
20Lakini watu hawakumsikiliza Mose. Baadhi yao walijibakizia chakula mpaka asubuhi. Lakini asubuhi chakula hicho kikawa kimeoza na kuwa na mabuu. Mose akawakasirikia sana watu. 21Basi, kila asubuhi walikusanya chakula kila mtu kiasi alichohitaji kula. Jua lilipopanda juu na kuwa kali, kile chakula kingine kiliyeyuka.
22Katika siku ya sita, Waisraeli walikusanya chakula hicho maradufu, pishi nne kwa kila mtu. Basi, wazee wote wa jumuiya ya Waisraeli walimwendea Mose, wakamweleza jambo hilo. 23Taz Kut 20:8-11 Mose akawaambia, “Hii ndiyo amri ya Mwenyezi-Mungu. Kesho ni siku rasmi ya mapumziko; ni Sabato takatifu ya Mwenyezi-Mungu. Basi, nendeni mkapike au mkachemshe kile chakula mnachohitaji leo, na chakula kitakachosalia kiwekeni mpaka kesho.” 24Basi, wakafanya hivyo na kukiacha chakula kingine mpaka kesho yake kama Mose alivyosema. Asubuhi yake waliona kwamba hakikuharibika wala kuwa na mabuu. 25Basi, Mose akawaambia, “Kuleni chakula hicho kilichosalia kwa sababu leo ni Sabato ya Mwenyezi-Mungu. Leo hamtapata chakula huko nje. 26Kwa siku sita mtakuwa mkikusanya chakula hiki, lakini siku ya saba ambayo ni Sabato hakitakuwapo.”
27Mnamo siku ya saba watu kadhaa walitoka kwenda kutafuta chakula, lakini hawakukipata. 28Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mpaka lini mtakataa kuzitii amri na Sheria zangu? 29Fahamuni kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nimewapa siku ya Sabato, ndiyo maana nikawapa chakula cha siku mbili mnamo siku ya sita. Basi, pumzikeni kila mtu nyumbani mwake; mtu yeyote asitoke katika siku ya saba.” 30Kwa hiyo, watu walipumzika siku ya saba.
31 Taz Hes 11:7-8 Waisraeli walikiita chakula hicho “Mana.”16:31 Mana: Neno la Kiebrania lasikika kuwa na maana ya “Nini hiki?” taz. 16:15. Kilikuwa kama mbegu za mtama mweupe na ladha yake ilikuwa kama mkate mwembamba uliotiwa asali. 32Mose akawaambia, “Hili ndilo agizo la Mwenyezi-Mungu: Chukueni kiasi cha pishi moja ya mana na kuiweka kwa ajili ya wazawa wenu, ili waweze kuona chakula nilichowalisha jangwani wakati nilipowatoa nchini Misri.”
33 Taz Ebr 9:4 Mose akamwambia Aroni, “Chukua gudulia utie ndani pishi moja ya mana na kuiweka mbele ya Mwenyezi-Mungu, iwe kwa ajili ya wazawa wenu.”
34Basi, Aroni akaiweka mana mahali patakatifu mbele ya sanduku la agano ili ihifadhiwe kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza Mose. 35Taz Yos 5:12 Waisraeli walikula mana kwa muda wa miaka arubaini, mpaka walipofika katika nchi iliyofaa kuishi, nchi iliyokuwako mpakani mwa Kanaani ambako walifanya makao yao. 36(Posho ya mana, kiasi cha pishi nne, ilikuwa sehemu ya kumi ya kipimo cha kawaida kiitwacho efa.)
Kutoka16;1-36

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: