Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 13 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo38....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu kwa Kutupa Nafasi na Kibali cha kuiona siku/wiki hii..
Tumsifu na Kumtukuza yeye Daima..

Msifuni Mwenyezi-Mungu! Jinsi gani ilivyo vizuri kumwimbia sifa Mungu wetu! Yeye ni mwema na astahili kuimbiwa sifa. Mwenyezi-Mungu anajenga tena mji wa Yerusalemu; anawarudisha Waisraeli waliokuwa uhamishoni. Anawaponya waliovunjika moyo; na kuwatibu majeraha yao. Anaamua idadi itakayokuwako ya nyota, na kuzipa zote majina yao. Bwana wetu ni mkuu, ana nguvu nyingi; maarifa yake hayana kipimo. Mwenyezi-Mungu huwakweza wanyenyekevu, lakini huwatupa waovu mavumbini. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu nyimbo za shukrani, mpigieni kinubi Mungu wetu! Yeye hulifunika anga kwa mawingu, huitengenezea nchi mvua, na kuchipusha nyasi vilimani. Huwapa wanyama chakula chao, na kuwalisha makinda ya kunguru yanapolia. Yeye hataki nguvu za farasi, wala hapendezwi na ushujaa wa askari; lakini hupendezwa na watu wamchao, watu wanaotegemea fadhili zake. Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee Yerusalemu! Umsifu Mungu wako, ee Siyoni! Maana yeye huimarisha milango yako, huwabariki watu waliomo ndani yako. Huweka amani mipakani mwako; hukushibisha kwa ngano safi kabisa. Yeye hupeleka amri yake duniani, na neno lake hufikia lengo lake haraka. Hutandaza theluji kama pamba, hutawanya umande kama majivu. Huleta mvua ya mawe kama kokoto na kwa ubaridi wake maji huganda. Kisha hutoa amri, maji hayo yakayeyuka; huvumisha upepo wake, nayo yakatiririka. Humjulisha Yakobo ujumbe wake, na Israeli masharti na maagizo yake. Lakini hakuyatendea hivyo mataifa mengine; watu wengine hawayajui maagizo yake. Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Asante Baba kwa wema na Fadhili zako,Ukaibariki siku/wiki hii na ukatubariki katika kazi zetu,Biashara,Masomo,Tuingiapo/Tutokapo,Vilaji/Vinywaji,Hatuaze ziwe nawe ee Mungu Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda,
Ukatutakase akili zetu Miili yetu,Utusamehe tulipo kwenda kinyume nawe Baba wa Mbinguni..Nasi tunaomba tuwezeshe kuwasamehe waliotukosea..
Utubariki na kutufanya  chombo chako tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Ukabariki kipato chetu kiingiacho na kitokacho Baba ukakiguse na kupata kibali chako katika matumizi yetu..
Tunarudisha shukrani kwako ee Mungu wetu,Sifa na Utukufu ni kwako..
Tuanajiachilia mikononi mwako Tukiamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu
Amina...!!!!!!
Muwe na Wakati mwema..Tuanze na Mungu.


Yuda na Tamari

1Wakati huo, Yuda alitengana na ndugu zake, akaenda kukaa na mtu mmoja Mwadulami, jina lake Hira. 2Akiwa huko, Yuda akamwona binti Shua, Mkanaani, akamwoa. 3Binti Shua akapata mimba akazaa mtoto wa kiume, Yuda akamwita Eri. 4Akapata mimba nyingine, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Onani. 5Kisha akapata mtoto mwingine wa kiume, akamwita Shela. Wakati Shela alipozaliwa, Yuda alikuwa Kezibu.
6Baadaye Yuda alimwoza mtoto wake wa kwanza Eri, kwa mwanamke aitwaye Tamari. 7Lakini Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mwovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; hivyo Mwenyezi-Mungu akamuua. 8Basi, Yuda akamwambia Onani, “Mchukue mke wa ndugu yako marehemu, kwani ndivyo inavyokupasa kufanya, upate kumzalia nduguyo watoto.” 9Lakini Onani alijua kwamba hao watoto wasingekuwa wake. Kwa hiyo, alipolala na mke wa nduguye, alimwaga chini mbegu ya uzazi, asije akampatia nduguye watoto. 10Tendo hilo likamwudhi Mwenyezi-Mungu, akamuua Onani pia. 11Ndipo Yuda akamwambia Tamari, mke wa mwanawe, “Rudi nyumbani kwa baba yako, ubaki mjane hadi mwanangu Shela atakapokua.” Yuda alihofu Shela naye asije akafa kama ndugu zake. Basi, Tamari akarudi nyumbani kwa baba yake.
12Kisha binti Shua, mkewe Yuda, akafariki. Yuda alipomaliza kufanya matanga akaondoka na rafiki yake Hira, Mwadulami, wakaenda Timna kwa wakata-manyoya ya kondoo wake. 13Tamari aliposikia kwamba baba mkwe wake alikuwa njiani kwenda Timna kukata manyoya ya kondoo wake, 14alivua mavazi yake ya ujane na kujifunika shela kisha akaketi penye lango la kuingilia Enaimu, kijiji kilichokuwa njiani kwenda Timna. Alifanya hivyo kwa vile aliona kwamba Shela alikwisha kuwa mtu mzima, lakini yeye Tamari hakuozwa awe mkewe.
15Basi, Yuda alipomkuta Tamari hapo, alimdhania kuwa mwanamke malaya, kwani alikuwa amejifunika uso. 16Hapo, bila kujua kwamba huyo alikuwa mke wa mwanawe, akamwendea pale kando ya njia, akamwambia, “Napenda kulala nawe.” Tamari akamwuliza, “Utanipa nini nikikubali?” 17Yuda akamjibu, “Nitakupa mwanambuzi kutoka kundi langu.” Tamari akamwambia, “Weka rehani kuthibitisha utaniletea huyo mwanambuzi.” 18Yuda akamwuliza, “Unataka nikupe nini kama rehani?” Naye akamjibu, “Nipe hiyo pete na kamba yake pamoja na hiyo fimbo unayoshika.” Basi, Yuda akampa vitu hivyo vyote, akalala naye. Tamari akapata mimba yake. 19Basi, Tamari akarudi nyumbani akavua ile shela aliyojifunika, akavaa tena mavazi yake ya ujane.
20Wakati Yuda alipomtuma yule rafiki yake, Mwadulami, ampelekee yule mwanamke mwanambuzi ili arudishiwe rehani aliyomwachia, Hira hakumpata. 21Hira akawauliza wenyeji wa Enaimu, “Yuko wapi yule mwanamke kahaba aliyekuwa kando ya njia karibu na hapa?” Wakamjibu, “Hapa hapajawa na mwanamke kahaba.” 22Basi, huyo rafiki akarudi kwa Yuda, akamwambia, “Sikumpata! Tena wenyeji wa huko wameniambia kwamba hapajawa na mwanamke kahaba yeyote huko.” 23Yuda akasema, “Acha avichukue vitu hivyo, la sivyo atatufanya tuchekwe. Wewe mwenyewe umeona kwamba nilimpelekea mwanambuzi, lakini wewe hukumpata.”
24Baada ya miezi mitatu, Yuda akapata habari, “Tamari, mke wa mwanao amekuwa kahaba, tena amepata mimba kwa kufanya ukahaba.” Basi, Yuda akaamuru, “Mtoeni nje achomwe moto!” 25Walipokuwa wakimtoa nje, Tamari akatuma ujumbe kwa baba mkwe wake, akisema, “Mwenye vitu hivi ndiye aliyenipa mimba. Kwa hiyo, nakuomba umtambue mwenye pete hii na kamba yake, na fimbo hii.” 26Yuda alivitambua vitu hivyo, akasema, “Tamari ni mwadilifu kuliko mimi. Ni kweli, maana sikumwoza kwa mwanangu Shela.” Tokea siku hiyo Yuda hakulala tena na Tamari.
27Wakati wa kujifungua kwake Tamari ulipofika, ikafahamika kuwa alikuwa na mimba ya mapacha. 28Basi, alipopata uchungu wa kuzaa pacha mmojawapo alitoa mkono nje, naye mkunga akaufunga kwa uzi mwekundu, akisema, “Huyu ndiye aliyezaliwa kwanza.” 29Lakini huyo mtoto alipourudisha mkono wake ndani, ndugu yake akazaliwa wa kwanza. Mkunga akasema, “Mbona wewe umepita kwa nguvu?” Kwa hiyo akaitwa Peresi. 30Baadaye ndugu yake akazaliwa akiwa na ule uzi mwekundu mkononi, naye akaitwa Zera.
Mwanzo38;1-30

Bible Society of Tanzania
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: