Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 7 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo34

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Asante Mungu wetu kwa siku hii njema ,Umetupa kibali chako na kutuchagua kuiona leo hii..Tunashukuru Baba wa Mbinguni kwa Neema/Rehema hii..Tunaomba ukaibariki siku hii na ukabariki Kazi zetu,Biashara,Masomo,Vyombo vya usafiri,Hatua zetu,Tuingiapo/Tutokapo,Vilaji/Vinywaji,Vyote tutavyogusa/tumia baba ukavitakase..
Kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo iliyomwagika kwa ajili yetu Ikatutakase Miili yetu,Akili zetu na kutuokoa..

Ndiyo maana Yesu pia,Kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe,Aliteswa na kufa nje ya mji.[Waebrania 13;12]


Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda..
Baba ukatusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakujua/kutojua,kuwaza na kunena..
Baba wa mbinguni ukawaponye/kuwaokoa wote wanaopitia Magumu/Majaribu,Vifungo vya mwovu,Shida/Tabu ukawaweke huru na ukaonekane kwenye maisha yao..

Wakumbukeni wale waliofungwa kana kwamba mmefungwa nao,Wakumbukeni wale wanaoteseka kana kwamba nanyi mnateseka kama wao[Waebrania 13;3]

Endeleeni kutembea katika njia iliyo nyoka,Ili kile kilicho lemaa kisiumizwe bali kiponywe[Waebrania 12;13]

Tunajiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni tukishukuru na kuamini wewe ni Bwana na mwokozi wetu..
Amina...!!!
Yesu Kristo ni  yuleyule jana,Leo na hata milele[Waebrania 13:8]
Tunawatakieni nyote neema ya Mungu[Waebrania13;25]


Simeoni na Lawi wanalipiza kisasi kwa ajili ya dada yao

1Siku moja, Dina, binti yake Yakobo na Lea, alikwenda kuwatembelea wanawake wa nchi hiyo. 2Basi, Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, aliyekuwa mkuu wa nchi hiyo, alipomwona Dina, akamshika, akalala naye kwa nguvu. 3Lakini Shekemu akavutiwa sana na huyo msichana, akampenda hata akaanza kumbembeleza. 4Kwa hiyo, Shekemu akazungumza na Hamori baba yake, akamwambia, “Tafadhali, niombee huyo msichana nimwoe.”
5Yakobo akapata habari kwamba Dina, bintiye, alikuwa amenajisiwa na Shekemu; lakini kwa kuwa wanawe walikuwa malishoni, alinyamaza mpaka waliporudi. 6Hamori, baba yake Shekemu, akaenda kwa Yakobo ili azungumze naye, 7na wakati huohuo watoto wa kiume wa Yakobo wakawa wanarudi nyumbani kutoka malishoni. Waliposikia hayo, vijana hao wakaona uchungu mwingi na kukasirika sana, kwa vile Shekemu alikuwa amewafanyia watu wa Israeli ovu hilo la kulala na binti ya Yakobo, maana jambo hilo lilikuwa mwiko.
8Lakini Hamori akawaambia, “Mwanangu Shekemu anampenda sana binti yenu. Basi, tafadhali mumruhusu amwoe. 9Acheni tuoane: Nyinyi mtatuoza binti zenu, nasi tutawaoza binti zetu. 10Kwa hiyo mtaishi pamoja nasi; mtakuwa huru katika nchi hii. Mtaishi humu, mfanye biashara na kujipatia mali.” 11Hali kadhalika, Shekemu akawaambia baba na ndugu zake Dina, “Tafadhali, mniwie radhi, nami nitawapeni chochote mtakachosema. 12Niambieni kiasi chochote cha mahari na zawadi, hata kikiwa kikubwa namna gani, nami nitatoa, mradi tu mnioze msichana huyu.”
13Basi, watoto wa kiume wa Yakobo wakamjibu Shekemu na baba yake Hamori kwa hila, kwa kuwa Shekemu alikuwa amekwisha mnajisi dada yao Dina. 14Waliwaambia, “Hatuwezi kumwoza dada yetu kwa mtu asiyetahiriwa. Kufanya hivyo ni aibu kwetu. 15Tutakubaliana nanyi tu kwa sharti hili: Kwamba mtakuwa kama sisi kwa kumtahiri kila mwanamume miongoni mwenu. 16Hapo ndipo tutakapowaoza binti zetu na kuwaoa binti zenu; tutaishi pamoja nanyi na kuwa jamaa moja. 17Lakini msipokubaliana nasi na kutahiriwa, basi, sisi tutamchukua binti yetu na kwenda zetu.”
18Pendekezo lao likawapendeza Hamori na mwanawe Shekemu. 19Kijana huyo hakusita hata kidogo kutekeleza sharti hilo, kwa vile alivyompenda binti wa Yakobo. Isitoshe, Shekemu ndiye aliyeheshimika kuliko wote nyumbani kwao.
20Basi, Hamori na mwanawe, Shekemu, wakaenda kwenye lango la mji, mahali pa mikutano, wakaongea na watu wao wakisema, 21“Watu hawa ni marafiki zetu. Tuwakaribishe waishi nchini mwetu na kufanya biashara, kwa sababu tunayo nchi ya kututosha sisi na wao pia; kisha tutaoa binti zao na kuwaoza binti zetu. 22Lakini wao watakubali kuishi nasi na tutakuwa jamaa moja kwa sharti hili: Kwamba tutamtahiri kila mwanamume miongoni mwetu kama wao walivyotahiriwa. 23Je, hamwoni kwamba mifugo yao na mali yao yote itakuwa mali yetu? Haya, tukubaliane nao ili wakae pamoja nasi.” 24Wanaume wote waliokusanyika penye lango la mji huo wakakubaliana na Hamori na mwanawe Shekemu. Kisha, wanaume wote wakatahiriwa.
25Siku tatu baadaye, waliotahiriwa wakiwa bado wana maumivu makali, watoto wawili wa Yakobo, Simeoni na Lawi, kaka zake Dina, walizitwaa panga zao, wakauvamia mji ghafla na kuwaua wanaume wote. 26Waliwaua kwa upanga Hamori na mwanawe Shekemu, wakamtoa Dina katika nyumba ya Shekemu, wakaenda zao. 27Baada ya mauaji hayo, watoto wengine wa kiume wa Yakobo waliingia mjini na kuuteka nyara mji huo, kwa sababu dada yao alikuwa amenajisiwa. 28Walichukua kondoo na mbuzi, ng'ombe, punda na chochote kilichokuwa mjini au shambani. 29Waliteka nyara mali yote, watoto na wanawake wote na chochote kilichokuwa majumbani.
30Basi, Yakobo akamwambia Simeoni na Lawi, “Nyinyi mmeniletea taabu kwa kunifanya nichukiwe na wakazi wa nchi hii ya Wakanaani na Waperizi. Mimi sina watu wengi, na kama wakikusanyika kunishambulia wataniangamiza mimi pamoja na jamaa yangu.” 31Hao ndugu wawili wakajibu, “Ana haki gani ya kumtendea dada yetu kama malaya?”
Mwanzo34;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: