Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 16 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi; Mwanzo21..


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Nimatumaini yangu mmeamka salama..Tunamshukuru Mungu kwa leo hii,Ametupa kibali cha kuiona tena..Wengi walitamani kuiona siku hii lakini wameshindwa,wengine ni wagonjwa wanashindwa hata kuinuka,Wengine hawana hata kauli, Sisi ni nani basi tumepewa hii Neema /Rehema ya kuwa Hai na wenye Afya na tushindwe kumuabudu Mungu,Kumshukuru Mungu,Kumsifu Mungu?
Tumempanini Mungu kwa uzima huu, sisi si kwamba ni wema sana zaidi ya wenzetu,si kwa nguvu/utashi wetu kuiona leo hii bali ni kwamapenzi ya Mungu wetu Muumba nchi na mbingu, Yeye ni mwingi wa Neema/Rehema, Yeye ni mtetezi wetu,Yeye asiye lala,Yeye ni mwokozi wetu,Yeye atupaye ridhiki zetu, Yeye awezae yote,Yeye ni mwamzo na yeye ni mwisho,Hakuna kama Yeye na hatokuwepo..
Mkabidhi Shida/Tabu zako,Magonjwa,Vifungo mbalimbali,Waliokata tamaa lipo Tumaini la kweli,Wafiwa yupo mfariji wa kweli,Wanaopitia Magumu/Majaribu yoyote mgeukie Mungu yeye anaweza..Akisema atakubariki hakuna wakupinga,Weka juhudi ya kumtafuta naye utamuona, Omba pasipokuchoka,Mwite na ataitika na kukutendea sawasawa na mapenzi yake.
Mungu Baba ukabariki Kuingia/Kutoka kwetu,Kazi,Biashara,Masomo,Vyombo vya usafiri na tutembeapo,Baba ukavitakase na damu yako vyote Tunavyoenda kuvitumia/kuvigusa..
Ukatuokoe na mwovu..Tunakuja mbele zako na kujiachilia mikononi mwako,Tukiamini wewe ni Bwana na mwokozi wetu..
Amina..!!!
Mbarikiwe.

Kuzaliwa kwa Isaka

1Mwenyezi-Mungu alimkumbuka Sara, akamtendea kama alivyoahidi. 2Basi, Abrahamu akiwa mzee, Sara akapata mimba, akamzalia mtoto wa kiume, wakati uleule Mungu alioutaja. 3Abrahamu akampa huyo mwanawe ambaye Sara alimzalia jina Isaka. 4Isaka alipotimiza umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri kama alivyoamriwa na Mungu. 5Abrahamu alikuwa na umri wa miaka 100 wakati mwanawe Isaka alipozaliwa. 6Naye Sara akasema, “Mungu amenipatia kicheko; yeyote atakayesikia habari hizi, atacheka pamoja nami.” 7Kisha akaongeza, “Ni nani angeweza kumwambia Abrahamu kwamba mimi Sara nitanyonyesha watoto? Tena nimemzalia mtoto wa kiume katika uzee wake!”
8Isaka akaendelea kukua, na siku alipoachishwa kunyonya, Abrahamu akafanya sherehe kubwa.

Hagari anafukuzwa
9Baadaye Sara alimwona Ishmaeli, mtoto wa Abrahamu aliyezaliwa na Hagari, Mmisri, akicheza na Isaka mwanawe. 10Basi, Sara akamwambia Abrahamu, “Mfukuzie mbali mjakazi huyu na mwanawe. Haiwezekani kabisa mtoto wa mjakazi kurithi pamoja na mwanangu Isaka.” 11Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa kuwa Ishmaeli pia alikuwa mtoto wake. 12Lakini Mungu akamwambia Abrahamu, “Usihuzunike kwa sababu ya mtoto huyu, wala huyo mtumwa wako wa kike. Lolote akuambialo Sara lifanye; kwa kweli wazawa wako watatokana na Isaka. 13Na kuhusu huyo mwana wa mjakazi wako, nitamfanya awe baba wa taifa kubwa kwa kuwa yeye pia ni mtoto wako.”
14Hivyo, asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari na kumtwika begani; akamfukuza pamoja na mwanawe. Hagari akaondoka, akawa anatangatanga nyikani Beer-sheba.
15Ikawa maji yalipomwishia katika kile kiriba, Hagari akamlaza mwanawe chini ya mti. 16Naye akaenda kando, akaketi umbali wa kama mita 100 hivi, akisema moyoni mwake, “Heri nisimwone mwanangu akifa.” Na alipokuwa ameketi hapo, mtoto akalia kwa sauti.
17Mungu akamsikia mtoto huyo akilia, na malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni, akamwambia, “Una shida gani Hagari? Usiogope; Mungu amesikia sauti ya mtoto huko alipo. 18Simama umwinue mtoto na kumshika vizuri mikononi mwako, kwani nitamfanya awe baba wa taifa kubwa.” 19Mungu akamfumbua Hagari macho, naye akaona kisima cha maji. Akaenda akajaza kiriba maji, akamnywesha mtoto wake.
20Mungu akawa pamoja na huyo mtoto, naye akaendelea kukua. Alikaa nyikani na akawa mpiga upinde hodari sana. 21Alikuwa akikaa katika nyika za Parani, na mama yake akamwoza mke kutoka nchi ya Misri.
Agano kati ya Abrahamu na Abimeleki
22Wakati huo, Abimeleki pamoja na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, alimwendea Abrahamu, akamwambia, “Mungu yuko pamoja nawe katika kila kitu unachofanya. 23Kwa hiyo niapie kwa jina la Mungu kwamba hutanifanyia hila mimi au watoto wangu au wazawa wangu. Kadiri mimi nilivyokuwa mwaminifu kwako, vivyo hivyo nawe uwe mwaminifu kwangu na kwa nchi hii unamokaa.” 24Abrahamu akasema, “Naapa.”
25Wakati huo Abrahamu alikuwa amemlalamikia Abimeleki juu ya kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamemnyanganya. 26Abimeleki akamwambia, “Mimi sijui nani aliyefanya hivyo; mpaka leo hii wewe hukuniambia; wala mimi sijapata kusikia habari hizi hadi leo.” 27Basi, Abrahamu akachukua kondoo na ng'ombe akampa Abimeleki nao wawili wakafanya agano baina yao. 28Abrahamu akatenga wanakondoo wa kike saba. 29Abimeleki akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini unawatenga hao wanakondoo wa kike saba?” 30Abrahamu akamjibu, “Hawa wanakondoo wa kike saba ninakupa kwa mkono wangu mwenyewe kama shahidi wangu kwamba mimi ndimi niliyechimba kisima hiki.” 31Kwa hiyo kisima hicho kikaitwa Beer-sheba, maana wote wawili walikula kiapo mahali hapo. 32Hivyo, wakafanya agano huko Beer-sheba. Abimeleki na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, akaondoka na kurudi katika nchi ya Wafilisti. 33Abrahamu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akamwabudu Mungu, Mungu wa milele. 34Abrahamu alikaa katika nchi ya Wafilisti muda mrefu.
Mwanzo21;1-34
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: